adsence

Pages

Wednesday, December 18, 2013

Barua ya Mwigamba yatua kwa msajili


Msajili wa Vyama vya Siasa,Jaji Francis Mutungi

Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, imethibitisha kupokea barua ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Akizungumza na paparazi wetu kwa njia ya simu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alithibitisha kupokea barua hiyo na kueleza kuwa ofisi yake inaifanyiakazi.
“Tumepokea barua ya Mwigamba, lakini siwezi kueleza kilichomo ndani yake kwa kuwa ndiyo tunaifanyia kazi…tutawaita wanahabari kuwaeleza hatua zilizochukuliwa na ofisi yangu,” alisema Jaji Mutungi.
Hivi karibuni katika mkutano na waandishi wa habari, Mwigamba ambaye amevuliwa madaraka yake yote ndani ya chama na wenzake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, aliwasilisha malalamiko yake kwa msajili.
Katika taarifa yake Mwigamba, amemuomba msajili kutoa mwongozo kuhusu anachodai kuwa ni mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya Chama kufuatia kipengele cha katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume na utaratibu. 
“Katiba ya Chadema ya mwaka 2004 kipengele 5.3.2 (c) inasomeka ifuatavyo kuhusu Muda wa Uongozi:Kiongozi aliyemaliza muda wa ungozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja,” alidai Mwigamba.
Hata hivyo, alisema Katiba ya chama ya mwaka 2006 kipengele cha 6.3.2 ( c) inayozungumzia muda wa uongozi unasoma: Kiongozi aliyemaliza muda wa ungozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi. 
“Sentensi kuhusu ukomo wa uongozi haipo. Ni kweli kuwa Marekebisho ya Katiba yalifanyika mwaka 2006, lakini hoja ya kubadili kipengele hicho haikuwepo na muhtasari zinaonyesha wazi kuwa kulikuwa hakuna mjadala wa kipengele hicho au kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi,” anadai. 
Novemba 22, mwaka huu, Kamati Kuu iliwavua madaraka viongozi hao na kuwataka wajieleze kwa maandishi ndani ya siku 14 baada ya kudaiwa kuhujumu chama kwa kuandika waraka wa siri unaodaiwa pamoja na mambo mengine, kuwadhalilisha viongozi wakuu wa Chadema.

No comments:

Post a Comment