Dodoma.Sakata la
wabunge waliochukua posho kwa ajili ya safari za mafunzo nje ya nchi na
kuacha kusafiri, limeingia hatua mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda kuwataka wazirudishe.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita mjini Dodoma na Mbunge wa
Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) wakati akichangia taarifa ya Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).
Keissy alisema baadhi ya wabunge wanapaswa kuchunguzwa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kuchukua posho za safari za
nje ya nchi lakini hawakwenda safari hizo.
Mbunge huyo alifafanua kuwa mbali na kutokwenda kabisa safari hizo,
lakini wapo ambao walikwenda na hawakukaa siku zote zilizopangwa.
“Tunawajua na wapo humu ndani,” alisema huku baadhi ya wabunge wakipaza
sauti wakitaka awataje, lakini yeye akasema siyo jukumu lake kuwataja
kwani Ofisi ya Bunge inawajibika kufanya hivyo.
Mbunge huyo alienda mbali na kudai mbunge mmoja alikatisha safari ya
kwenda Marekani na kuamua kwenda Dubai kwa safari binafsi ambayo
haikuwepo katika ratiba ya ziara hiyo ya mafunzo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema wabunge wanane walichukua
posho ya safari ya kati ya Sh5 milioni na Sh6 na Spika amewaandikia
barua akiwataka warudishe fedha hizo.
Majina ya wabunge hao tunayo, lakini kwa sababu za maadili ya uandishi
wa habari, gazeti hili halitaweza kuwataja kwa kuwa hawakupatikana ili
kujibu tuhuma hizo kama maadili yanavyoelekeza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana,
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa Spika ameshaliona jambo
hilo na kulichukulia hatua za kiutawala.
“Spika amewaandikia barua akiwataka kurejesha fedha zote za safari
ambazo hawakwenda. Ni lazima wazirudishe hakuna namna,” alisema Joel
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge.
Alipoulizwa kuhusiana na majina yao na kiasi walichochukua, Joel alisema
hilo ni jambo la kiutawala na kwamba Spika ndiyehuarifiwa na kamati
kuhusiana na wabunge ambao hawakusafiri.
“Spika ndiye anayearifiwa na wenyeviti wa kamati husika juu ya wabunge
waliosafiri na wasiosafiri kwa sababu wao ndiyo wanapanga safari na sisi
tunawapa posho,” alisema.
Akizungumzia malalamiko ya wabunge juu ya baadhi ya wabunge wasiofika
bungeni kusaini ili wapate posho ya kikao, Joel alisema tatizo hilo
limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Lilikuwepo lakini limepungua kwa kiasi kikubwa baada ya kugundua
wakifika kwenye malipo majina yao waliosainiwa yamekatwa,” alisema Joel.
Alipoulizwa kuhusiana na tatizo hilo la kupokea posho za safari za nje
ya nchi bila kwenda, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani bungeni,
Tundu Lissu alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo.
“Lakini muhimu hapa ni Bunge kuandaa utaratibu wa kurejesha mrejesho wa
jinsi walivyozitumia na hapo ndipo watagundulika wabunge wanaosafiri
kweli na muda waliokaa mahali husika,” alisema Lissu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye anatajwa
kuwemo kwenye orodha ya wabunge waliopokea posho bila kusafiri, alikiri
na tayari alishamuandikia barua Katibu wa Bunge akimueleza kwamba
hakusafiri na kuomba utaratibu wa kurejesha fedha hizo.
Nasari alisema yeye alikuwa Jimboni kwake kwa shughuli za wananchi wake,
hivyo hakuweza kusafiri na suala hilo alilifikisha mapema kwa Katibu
ili ampe maelekezo namna ya kurejesha fedha hizo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment