KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kutoa kauli ya kukatisha tamaa.
  Simbachawene,  juzi alitoa kauli ya serikali ya kupandisha  bei ya 
umeme kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lilivyoomba hivi  
karibuni kutaka kuongeza gharama za nishati hiyo kwa asilimia 68.
  Alisema  ni ukweli usiopingika kuwa hata TANESCO ikiongeza gharama za 
umeme hadi kufikia  sh 800 kwa uniti bado bei hiyo itaendelea kuwa nafuu
 ukilinganisha na  gharama za kununua mafuta ya taa.
  Simbachawene  alitoa tahadhari kwamba endapo kuna mwananchi yeyote 
atakayeona gharama za  umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari 
au akae gizani.
  Akizungumza  na Tanzania Daima Jumatano jana, Mkurugenzi wa Kituo 
hicho, Dk. Helen  Kijo-Bisimba, alisema kuwa kauli hiyo inaweza 
kusababisha vurugu kutokana na  suala la umeme kumgusa kila Mtanzania.
  Alisema  kuwa hivi sasa viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kuudhi ambazo ni hatari kwa  ustawi wa taifa.
  “Tunakumbuka  kauli za kuudhi zinavyozidi kushamiri wakti ule 
aliyekuwa Waziri wa Fedha  Basili Mramba alipowaambia Watanzania 
wajifunge mikanda kubana matumizi hata  ikibidi kula majani watakula, 
lakini ndege ya rais lazima inunuliwe; akaja  Waziri wa Ujenzi John 
Magufuli aliyewaambia wakazi wa Kigamboni kuwa kama  hawawezi kulipa 
ongezeko la nauli mpya basi wajifunze kupiga mbizi, ili kuvuka  kwa 
kuogelea, wanaporudi vijijini au wazunguke kupitia Kongowe sasa hii ya  
vibatari!”alisema.
  Alisema  kuwa ni muhimu viongozi wakahakikisha wanatoa kauli zilizo na hekima ili  kuepusha migogoro.
  Mkurugenzi  huyo alisema kuwa baada ya serikali kupandisha gharama hizo, muathirika mkubwa  ni mwananchi wa chini.
  Alisema  kuwa wamiliki wa viwanda wanachoangalia ni faida hivyo 
kupanda kwa bei ya umeme  kutasababisha gharama za bidhaa kuzidi kuwa 
juu zaidi.
  “Nchi  za wenzetu hakuna jambo linaloweza kufanywa bila kushirikisha 
wananchi lakini  hapa kwetu wanaamua tu na mbaya zaidi wanakuja na kauli
 za kuudhi na kukatisha  tamaa kwa kuwa Watanzania ni wapole,” alisema.
  Dk.  Bisimba alisema kuwa ni lazima wafahamu kuwa upole wa Watanzania 
utafikia  kikomo na hiyo inaweza kusababisha hatari kwa taifa.
  Wiki  hii wadau mbalimbali wa umeme likiwamo Shirikisho la Wenye 
Viwanda Tanzania  (CTI) na Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za 
Nishati na Maji (EWURA CCC),  walipinga maombi ya Shirika la Umeme 
Tanzania (TANESCO) ya kuongeza gharama za  umeme kwa asilimia 67.8.
  Walisema  ongezeko hilo ambalo limelenga zaidi viwanda vikubwa na vya 
kati litasababisha  kupanda kwa bei za bidhaa za viwandani.
  Mjumbe  wa Bodi ya CTI, Samuel Nyantahe, alisema kabla TANESCO 
haijapandisha gharama  hizo ingekusanya madeni yote na kuziba mianya ya 
wizi wa umeme.
  
  Naye  Mjumbe wa CCC Thomas Mnunguli, alisema ongezeko hilo ni kubwa na
 linakosa  uhalali hivyo TANESCO ijitathmini na kujipanga upya na ilenge
 kutoa huduma bora  na nafuu.
-Tanzania Daima
-Tanzania Daima
 

 
No comments:
Post a Comment