
MASHITAKA
 11 dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, 
yamebainisha kuwa kosa kubwa la kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya 
kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Chanzo chetu cha habari kilichoona mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa 
washitakiwa, kimebainisha kuwa makosa saba kati ya makosa 11, yanahusu 
kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa.
“Ukiona hayo mashitaka yenyewe ndugu yangu, yanajirudia rudia na 
kuzunguka katika kosa moja la nia ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa 
Taifa… angalia kosa la kwanza, kosa la tatu, tano, sita nane na tisa, ni
 kama vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.
“Hata hivyo kwa jinsi mgawanyiko ulivyo ndani ya chama sasa, 
nakuhakikishia hawa jamaa (Zitto, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba), 
watarudishwa katika nyadhifa zao na hakuna atakayeadhibiwa,” alisema 
mtoa taarifa wetu.
Alinukuu kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga 
Baregu aliyehoji kama makosa wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi
 cha kuyeyusha mema aliyoyafanya katika chama. “Si umesikia akina Baregu
 wakizungumza? Kwa mashitaka yale nakuhakikishia kitakachofanyika ni 
kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema mtoa habari wetu.
Kosa la kwanza kwa Zitto, Dk 
Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya Chama inayokataza 
kukashifu chama, kiongozi au mwanachama yeyote. Katika maelezo ya kosa 
hilo, akina Zitto wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe, 
Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
Moja ya madai katika mashitaka hayo, ni kilichoandikwa katika Mkakati wa
 Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe amekuwa akinunua vifaa vyote vya chama nje 
ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo haihojiwi popote. Wanadaiwa
 pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni mdhaifu kwa kumruhusu Mbowe 
kuingilia shughuli za kiutendaji.
Zitto na wenzake wanadaiwa katika kosa la pili, kutokuwa wawazi 
na wa kweli wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na 
udanganyifu kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII. 
Katika kosa la tatu, wanadaiwa 
kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao halali na 
utaratibu wa ngazi zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).
Katika kosa la nne, akina Zitto
 wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au 
ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama, miongoni mwa 
jamii, kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo wanadaiwa kwenda kinyume na 
kipengele cha 10.1 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Akina Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa kujihusisha na vitendo
 vya kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa chama au wanachama,
 kinyume na kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Katika kosa la sita ambalo mtoa habari wetu alisema ndio kubwa, 
Zitto na wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea 
uenyekiti wa Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi 
hiyo.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kinyume na kifungu 2.C cha Muongozo wa 
Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na 
Serikali wa 2012.
Zitto na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa kutengeneza 
mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikishia 
ushindi kinyume na kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania Uongozi. 
Katika kosa la nane, Zitto na 
wenzake wanadaiwa kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye 
kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti kinyume na kifungu 2 
(E) cha Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika kosa hilo, kumewekwa maelezo ya ziada kuwa kosa hilo 
linaunganishwa na kosa la kwanza ambalo washitakiwa wanadiwa kuwakashifu
 Mbowe, Dk Slaa na Lema.
Kosa la tisa, akina Zitto wanadaiwa 
kujihusisha na upinzani dhidi ya chama na makundi ya majungu ya 
kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa chama, kinyume 
na kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za Uendeshaji.
Kosa la kumi linamhusu Zitto peke 
yake, ambapo anaidaiwa kukashifu chama na kiongozi wa chama nje ya Bunge
 kinyume na kifungu 2 C (B), kikisomwa pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni 
za Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.
Katika hilo Zitto kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa chama yaani 
Dk Mkumbo na Mwigamba na mtu mwingine ambaye hajajulikana, wanadaiwa 
kusambaza waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mkakati huo, unadaiwa kukashifu chama na/ au viongozi wake wakuu kama ilivyoelezwa katika kosa la kwanza, tatu, nne na nane.
Mwisho katika kosa la 11, Zitto
 na wenzake wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya chama kinyume na 
kanuni ya 3 F ya Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Bunge.
CHANZO: HabariLeo
 

 
No comments:
Post a Comment