Stori: Makongoro Oging’
DUNIA haiishi vituko! Chacha Makenge (36) mzaliwa wa Kijiji cha Kisangula, Mtukula, Serengeti mkoani Mara anaishi jijini Dar lakini ndani ya handaki aliloligeuza chumba kwa miaka minne sasa, ni ajabu lakini ni kweli.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni nje ya handaki hilo lililopo mita chache kutoka majengo ya biashara ya Mlimani City, Makenge alisema alichukua uamuzi huo baada ya rafiki yake (jina linahifadhiwa) kumchomea nyumba na kuteketeza samani zote.
“Ilikuwa mwaka 2009 mwanzoni rafiki yangu huyo ndiye alinipa sehemu ya kiwanja chake nijenge nyumba. Nikawa naishi hapo huku nikiendelea na shughuli zangu za kila siku.
“Siku moja akabadili mawazo, akanitaka nihame katika eneo lake bila kunipa sababu, nilimwomba anipe muda nitafute pa kwenda.
“Julai 2009 akaja na polisi, akanikamata na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Stakishari, nilipowauliza kosa langu, hawakunieleza.
“Baada ya siku mbili majirani walikuja kuniona na kuniambia kwamba nyumba yangu imechomwa moto na kila kitu kilichokuwa ndani kimeteketea, aliyefanya hivyo ni rafiki yangu. Nilijisikia vibaya sana.
“Siku iliyofuata majirani walikuja tena kituoni wakaniwekea dhamana. Nilipofika kwangu nilikuta majivu tu, iliniuma sana, nililia lakini sikupata ufumbuzi. Kwa vile nilikuwa sina pa kwenda ilibidi niwe nalala palepale nilipochomewa nyumba nikisaidiwa chakula na majirani.
“Siku iliyofuata, saa nne usiku nilivamiwa na watu wanne, wakiwa na mapanga na marungu, nilipambana nao mpaka wakaondoka. Kesho yake nilikwenda kwa mwenyekiti wetu wa serikali ya mtaa, Jumanne Malima kumweleza yaliyonipata, alisikitika, akaniandikia barua kwenda Polisi Stakishari.
“Nilipofika kituoni sikusikilizwa, badala yake walinikamata tena na kuniweka ndani wakidai kwamba nimefunguliwa kesi ya kumjeruhi mtu kwa panga. Hawakukubali niwekewe dhamana.
“Julai 31, 2009 nilifikishwa Mahakama ya Mwanzo Ukonga na baadaye nilipelekwa Mahabusu ya Gereza la Keko, nikawa napelekwa mahakamani hadi Septemba mwaka huo ambako nilihukumiwa kwenda jela miezi 9.
“Nilitumikia maisha ya jela hadi Desemba 10, 2009 nikatolewa kwa msamaha wa Rais Jakaya Kikwete. Nilikwenda kuishi kwa ndugu zangu huku wakifuatilia sababu ya kufanyiwa vitendo hivyo bila mafanikio.
“Maisha ya kwa ndugu hayakunifurahisha kwani hata wao walikuwa na majukumu mengi, niliamua kuendelea na kazi zangu za sanaa pia utunzaji wa mazingira na bustani kwa watu wakawa wananilipa fedha.
“Ndipo nilipoamua kutafuta sehemu iliyotulia ili niweze kuishi, nikapata hapa, ni jirani na Mlimani City. Nilichimba handaki kubwa kama unavyoliona, kwa chini kuna kitanda ninacholalia.
“Kwa hakika hapa sipati shida, wala kelele. Kwanza ni tulivu sana, nimefikia hatua ya kuishi kama mnyama kutokana na mateso na bugudha nilizopata, wengi hawajui nilipo, nipo katika pori hili kwa miaka minne sasa,”alisema Makenge.CHANZO GPL
No comments:
Post a Comment