MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kwa mara nyingine ameingia matatani baada ya kushindwa kesi iliyofunguliwa na mfanyabiashara raia wa Afrika Kusini.
Katika kesi hiyo, Zitto alituhumiwa kutoa madai kupitia tovuti yake www.zittokabwe.wordpress.com kuwa mlalamikaji, Moto Mabanga alitoa rushwa ya mabilioni ya fedha kwa maofisa wa Serikali ya Tanzania ili kufanikisha kampuni ya Ophir Energy kupata vitalu vitatu vya gesi mkoani Mtwara kati ya mwaka 2004/2005.
Katika kesi hiyo ya madai Namba 153 ya 2013 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo pamoja na mambo mengine alidai kulipwa fidia ya Dola za Marekani milioni 5 ambazo ni sawa na Sh bilioni 8 za Tanzania.
Katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Sundi Fimbo, Novemba 21 mwaka huu bila Zitto kuwapo, Mahakama ilijiridhisha kuwa maneno yaliyoandikwa kwenye tovuti binafsi ya Zitto na kwenye mitandao ya jamii yalimkashifu mlalamikaji na mlalamikiwa ameshindwa kuyathibitisha.
Mahakama hiyo imemtaka Zitto kuomba radhi kwenye tovuti yake na mitandao ya jamii ambako aliandika kashfa dhidi ya mfanyabiashara huyo.
Pia imemuamuru mlalamikiwa pamoja na washirika wake kuacha kwa njia yoyote ile kuendelea kuandika na kusambaza habari zenye kumkashifu mlalamikaji.
Mwanasiasa huyo kijana ambaye katika siku za karibu amekumbwa na misukosuko ya kisiasa, pia ameamriwa kumlipa mlalamikaji jumla ya Sh milioni 3 kutokana na madhara yaliyotokana na kashfa husika.
Awali, mlalamikaji alitaka kulipwa Dola za Marekani milioni 5, lakini akashindwa kuithibitishia Mahakama ni jinsi gani alipata hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kashfa hiyo. Pia Zitto ametakiwa kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Alipoulizwa jana kama anakubaliana na hukumu hiyo au anakusudia kukata rufaa, Zitto alijibu kwa ufupi; “Sijaona hukumu wala sijawahi kufika mahakamani.”
Julai mwaka jana, Mabanga alifikisha malalamiko mahakamani akidai Zitto ameandika taarifa zenye kumkashifu kwa kumhusisha na utoaji mkubwa wa rushwa.
Mbali na kujihusisha na biashara sehemu mbalimbali duniani, Mabanga amekuwa akitumika kama kiunganishi kati ya wawekezaji wakubwa na Serikali mbalimbali ikiwamo Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika madai yake, aliitaka Mahakama kumuamuru Zitto kutoka uthibitisho dhidi ya madai ya kuwapa rushwa maofisa wa Serikali katika mchakato wa kupata vitalu vya gesi wa kampuni ya Ophir Energy.
Pia aliiomba Mahakama kutamka kuwa maneno yaliyoandikwa na Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha kwenye tovuti yake na mitandao ya jamii si ya kweli bali ni kashfa.
Wakati hali ikiwa hivyo, wiki mbili zilizopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilimvua nyadhifa zote Zitto Kabwe ikiwamo ile ya Naibu Katibu Mkuu.
Katika mkutano wa Kamati Kuu ya Chadema uliofanyika Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu, alisema Zitto na wenzake wamebainika kukihujumu chama kwa kuanzisha mpango unaoitwa Mkakati 2013 ukilenga kukisambaratisha chama hicho, ili kuwaondoa madarakani Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake.
Wengine waliovuliwa nyadhifa zao ni pamoja Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, ambapo walipewa siku 14 wajieleze kimaandishi kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kinidhamu ikiwamo kuvuliwa uanachama.
-Mtanzania
No comments:
Post a Comment