Imebainika kwamba sababu ya shambulizi la risasi lililotokea Ilala Bungoni, Dar es Salaam Jumanne iliyopita na kusababisha vifo vya watu watatu, ni wivu wa mapenzi uliopindukia.
Akizungumza nyumbani kwao Ilala Bungoni jana, 
mmoja wa majeruhi ambaye ndiye aliyekuwa kiini cha shambulizi hilo, 
Christine Newa alisema si kweli kwamba sababu ya mchumba wake, Gabriel 
Munisi kuwashambulia na kuwajeruhi kwa risasi yeye na mama yake mzazi, 
Ellen Eliezer na kumuua mdogo wake wa kike, Alpha Newa ni kutokana na 
kusaliti uchumba wao.
  
Awali, ilidaiwa kwamba sababu ya shambulizi hilo 
ni Christine kumkataa Munisi, (ambaye pia alijiua baada ya kufanya 
mauaji hayo) na kuchumbiwa na rubani wa ndege, marehemu Francis Shumila 
ambaye pia alifariki katika tukio hilo... “Kwanza Shumila hakuwa mchumba
 wangu kama ilivyoelezwa. Alikuwa shemeji yangu, mume wa dada yangu 
Caroline Newa. Pia hakuwa rubani wa ndege, bali nahodha wa meli.”
  
Alisema amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na 
Munisi katika kipindi kisichofikia mwaka mmoja lakini sehemu kubwa ya 
maisha yao ikitawaliwa na misuguano iliyowafikisha polisi mara kadhaa.
  
Alisema katika kipindi cha uhusiano wao marehemu 
Munisi alikuwa akimpiga, akimkataza kufanya kazi, kusoma na alikuwa na 
wivu uliopindukia.
Christine kuona hivyo, aliamua kufanya mipango ya 
kwenda kusoma katika Visiwa vya Cyprus kimyakimya pasi na kumuaga, jambo
 ambalo alisema lilimkera mchumba wake huyo na kuweka kisasi.
  
“Nikiwa huko, Munisi alitafuta mawasiliano hadi 
akayapata na tukawasiliana na siku niliporejea alikuja kunipokea uwanja 
wa ndege lakini cha ajabu, alinikataza kwenda nyumbani na badala yake 
akanipeleka moja kwa moja hadi Mwanza eneo la Kitangiri,” alisema na 
kuongeza: “Tukiwa njiani kuelekea Mwanza, katika maeneo ya Singida, 
alisimamisha gari akaniambia nishuke, akatoa bastola na kuniuliza kwa 
nini niliondoka bila ya kumuaga. Je, nataka kumuacha?”
  
Alisema alimwomba msamaha na kuendelea na safari 
yao. Anasimulia kwamba baada ya kufika Mwanza, alimpora simu zake zote 
na kumfungia ndani kwa zaidi ya wiki mbili hadi alipopanda kwenye 
dirisha na kuomba msaada kwa majirani na kuwapa namba za simu za ndugu 
zake ili wamsaidie kuwapa taarifa.
  
Ndugu zake walianza mchakato wa kuwasiliana na 
polisi hatua iliyofanikisha msichana huyo kurudishwa Dar es Salaam... 
“Hata hivyo niliondoka na khanga na fulana tu. Vitu vyote niliviacha 
huko.”
Baada ya kurudi Dar es Salaam, anasema Munisi naye
 aliamua kumfuata lakini safari hii alifikia katika Hoteli ya MM 
iliyotenganishwa na ukuta wa nyumba yao na akawa anafuatilia nyendo za 
familia hiyo.
  
“Alikuwa ananitumia meseji kwamba amemuona dada 
Caro, mama na Alpha na wakati mwingine anasema ameniona mimi mpaka nguo 
tulizovaa, tukaanza kupata na wasiwasi,” alisema.
  
Wasiwasi huo ulitokana na historia ya maisha yao 
ya Mwanza na pia tishio ambalo anadai kwamba Munisi aliwahi kulitoa 
kwamba atahakikisha anaiteketeza familia yote kuanzia Goba anakoishi 
mama yake (Ellen), Zanzibar anakoishi mdogo wake (marehemu Alpha) na 
hapo Ilala.
Anasema walikwenda polisi lakini walielezwa kwamba hayo ni masuala madogo ya mapenzi na kwamba yatamalizwa kifamilia.
  
Siku ya tukio Christine alikuwa akitoka kwenda 
uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kurudi shuleni Cyprus ndipo Munisi 
alipotokea na kuanza kumrushia Shumila risasi na baadaye Alpha kisha 
mama na yeye kabla ya kujiua.
  
Akizungumzia tukio hilo, Caroline alisema mumewe 
alitabiri kifo chake kabla kwani baada ya kusikia vitisho vya Munisi, 
alimtoa shaka Christine akimwambia kwamba atamlinda hata ikibidi 
kupoteza maisha yake, jambo ambalo lilidhihiri.
  
Alisema mama yake amepata nafuu na ameruhusiwa 
kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa na mazishi
 ya mdogo wake, Alpha ambaye ameacha mtoto mwenye umri wa miezi minane, 
yamepangwa kufanyika Jumamosi Goba, Dar es Salaam.
  
Alisema mipango ya mazishi ya mumewe inafanywa huku akidokeza kwamba huenda akasafirishwa kwenda Mombasa.
-Mwananchi
-Mwananchi
 

 
No comments:
Post a Comment