Jana jioni, Dk Slaa alifanya mkutano wa hadhara Mjini Manyovu na kusema 
kuwa hatishwi na waandamanaji wala vitisho vya kuuawa na kusisitiza kuwa
 ataendelea na ziara yake kama kawaida hadi Kigoma Mjini.
Awali, akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji 
cha Malumba wilayani Kasulu, juzi Dk Slaa alisema siyo mara yake ya 
kwanza kutishwa na kusema analindwa na Mungu.
Licha ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanachama wanaodai 
kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake zote, aliyekuwa Naibu 
Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe alisema ataendeleza kazi kuimarisha uhai 
wa chama kama ratiba ilivyopangwa.
Akiwa katika jimbo hilo linaloongozwa na Zitto, Dk Slaa atatembelea 
Vijiji vya Nyarubanda na Kidahwe na kufanya mikutano ya hadhara 
inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa siasa nchini kutokana na mzozo huo 
uliokikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini, Ally Kisala alisema 
maandalizi ya mikutano hiyo yamekamilika na kwamba hakuna hofu yoyote ya
 kutokea vurugu katika mikutano hiyo.
“Tumedhibiti aina yoyote ya vurugu iliyokusudiwa licha ya kuwapo baadhi 
ya watu wanaotamani hayo yatokee kwa lengo lao binafsi, sambamba na 
kunufaisha masilahi ya makundi binafsi, lakini hayatatokea,” alisema.
Juzi, wanachama na wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto 
waliandamana kupinga ziara ya Dk Slaa katika jimbo lao kupinga hatua ya 
kumvua mbunge wao madakara.
“Tunaamini mikutano yote ya kesho (leo Jumanne) itafanyika vizuri na 
watu watapata ujumbe kutoka kwa Katibu Mkuu wetu (Dk Slaa), na pengine 
wale wanaopiga kelele na kutaka kuleta mgawanyiko ndani ya chama 
watapata fursa ya kuujua ukweli wa mambo ndani ya chama.
“Vita yetu si kukigawa chama, bali ni kuhakikisha tunaingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Kisala.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia Makunja alisema jeshi 
lake limejipanga kuhakikisha usalama unakuwapo katika ziara hiyo.
“Tunawajibika kuhakikisha usalama unakuwa vizuri na kila jambo 
linaendelea kama lilivyopangwa. Mwito wangu kwa viongozi, wanachama na 
wapenzi wa Chadema ni kuhakikisha wanamaliza tofauti zao mapema ili 
kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, hatupendi kuona askari wetu 
wakilazimishwa kutumia nguvu kudhibiti hali ya usalama,” alisema 
Makunja.
Dk Slaa anatarajia kukamilisha ziara yake mkoani Kigoma keshokutwa kwa 
kuzungumza na viongozi wa mkoa kabla ya kwenda Tabora ambako atafanya 
kikao cha viongozi wa Kanda ya Magharibi inayounganisha Mikoa ya Kigoma,
 Tabora na Katavi.
Mkutano wa Bavicha Dar
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema chama hicho hakiwezi 
kuwavumilia watu wanaoendeleza ghasia katika mikutano ya Dk Slaa huko 
Kigoma.
Akizungumza katika Kongamano la Miaka 52 ya Uhuru lililoandaliwa na 
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Dar es Salaam jana, Lissu 
alisema: “Naomba niseme suala la Zitto Kabwe ambalo kama wiki tatu hivi 
limekuwa likizungumzwa sana. Chadema siyo chama cha mtu mmoja, sisi 
tunaangalia nidhamu, tutaendelea kuwafukuza watu wa aina kama hiyo ambao
 ni wasaliti na watovu wa nidhamu kwenye chama.”
Mbali ya Lissu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema huku akishangiliwa
 alisema, Chadema ina nguvu ya kushika dola mwaka 2015 hivyo lazima iwe 
na watu wenye nidhamu na si wapenda madaraka.
“Ni vyema ikafahamika kuwa kilio chetu siyo madaraka ni mabadiliko. 
Hivyo sisi hatuwezi kuwafumbia macho watu ambao hawakitakii mema 
Chadema... uongozi siku zote ni changamoto, hivyo kufanyika kwa 
mabadiliko ni kitu cha lazima.”
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Tukiwa 
tunasherehekea miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni vyema vijana 
tukatafakari kitu gani kimefanyika kwa miaka yote hiyo.
“Miaka 52 ya Uhuru tumeshuhudia ufisadi, rushwa na masuala mengine ya 
kuwakandamiza wananchi. Kitu cha msingi ni kupambana na mambo haya. Ni 
wajibu wetu vijana kuamka na kuchukua hatua ya kulitetea Taifa letu.”
Akifungua kongamano hilo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema tukiwa 
tunaadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara chini ya uongozi wa 
CCM, hakuna mabadiliko yoyote na kwamba ahadi ya maisha bora kwa kila 
Mtanzania haipo.
Mwananchi
 
 
No comments:
Post a Comment