Kwa ufupi
Ni kuhusu wanachama wa chama hicho kuhudhuria mkutano wa amani.
Arusha/Shinyanga/Dar.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wametofautiana kauli kuhusu wanachama na wafuasi wao kuhudhuria mkutano wa amani kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha leo.
Wakati Dk Slaa akiwahamasisha wahudhurie, Lema aliwataka wasihudhurie kwa sababu Jiji hilo lina matatizo mengi yanayohusiana na uvunjifu wa amani na bado Serikali haijayapatia ufumbuzi.
Mkutano huo umeandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi akitaka uvishirikishe vyama vyote vya siasa, viongozi wa dini na wananchi wa Jiji la Arusha kwa ujumla.
Akiwa kwenye Uwanja wa TCD Wilayani Kahama, Dk Slaa alisema kuwa ni nafasi kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa vyama vya siasa kuhudhuria mkutano huo kwa kuwa si wa chama kimoja bali ni wote.
“Napongeza hatua ya kuitisha mkutano, amani inatafutwa kwa njia mbalimbali, sasa hili ningependa kuona wote wanashiriki,” alisema.
Wakati Dk Slaa akisema hayo, Lema aliwahamasisha wanachama na wafuasi wa Chadema kutoshiriki mkutano huo hadi hapo Serikali itakapotoa majibu ya msingi ya chanzo cha kuibuka migogoro katika Jiji la Arusha.
Alisema chanzo cha migogoro ya Arusha ni uchaguzi wa meya ambao CCM ilicheza rafu kwa kumwingiza Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda kuwa mmoja wa madiwani wa jiji hali ya kuwa ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga.
Matukio mengine, alisema: “Kuna mauaji ya Januari 5, mwaka 2011, kuna mauaji ya Soweto yote haya tuliomba tume huru sasa leo wanataka mkutano wa amani hili hatukubali kwani ni mchezo mchafu...nawaomba wakazi wa jiji kutohudhuria mkutano huu,” alisema Lema.
Wakati huo huo, Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Bavicha) limesema siku ya maadhimisho ya uhuru, Desemba 9, mwaka huu litafanya kongamano kujadili miaka 52 tangu Tanzania kupata uhuru imefikia wapi.
Pia, Bavicha imesema siku hiyo haitajali kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa na kupigwa mizinga ila wao watafanya kongamano na Watanzania wenyewe ndiyo watapima wapi pakwenda kusikiliza vitu vinavyojadiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratias Munishi alisema viongozi wakuu wa Chadema watazungumza kwenye kongamano hilo na kwamba kila Mtanzania anaruhusiwa kushiriki ili kujua muelekeo wa nchi yake.Mwananchi: Dk Slaa, Lema wasigana kauli.
No comments:
Post a Comment